Ruka hadi kwenye maudhui
Beta

Uzi bado haujatafsiriwa kikamilifu kwa Kiswahili. Kile ambacho bado hakijatafsiriwa kinaonyeshwa kwa Kiingereza.

1 Samweli 21

Sura hii ni sehemu ya: David en Saul

1Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?” 2Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi yako wala maagizo yako!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia tukutane mahali fulani. 3Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.” 4Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.” 5Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?” 6Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwepo mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonyesho iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za Bwana na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa. 7Basi siku hiyo palikuwepo na mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za Bwana; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachunga wanyama wa Sauli. 8Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.” 9Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungiwa katika kitambaa nyuma ya kisibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.” Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.” 10Siku ile Daudi akamkimbia Sauli na kwenda kwa Akishi mfalme wa Gathi. 11Lakini watumishi wa Akishi wakamwambia, “Je, huyu si ndiye Daudi mfalme wa nchi? Je, huyu si ndiye yule ambaye wanaimba katika ngoma zao wakisema: “‘Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake’?” 12Daudi akayaweka maneno haya moyoni naye akamwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi. 13Basi akajifanya mwendawazimu mbele yao; naye alipokuwa mikononi mwao, alitenda kama kichaa, akikwaruza kwa kutia alama juu ya milango ya lango na kuachia udelele kutiririka kwenye ndevu zake. 14Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni mtu huyu! Ana wazimu! Kwa nini mnamleta kwangu? 15Je, mimi nimepungukiwa na wenda wazimu kiasi kwamba mmeniletea mtu huyo hapa aendelee kufanya hivi mbele yangu? Je, ilikuwa ni lazima mtu huyo aje nyumbani kwangu?”

Namba za mistari hufuata tafsiri uliyochagua, na katika sura chache zinaweza kutofautiana kwa mstari mmoja.

Urahisi wa kusoma

Chagua kinachokusaidia. Chaguo lako linahifadhiwa kwenye kifaa hiki.

Ukubwa wa maandishi

Unapendelea mipangilio ya kifaa chako mwenyewe (kukuza, kisoma skrini, hali ya giza)? Inafanya kazi hapa pia.